RAIS DK. MAGUFULI AZINDUA MPANGO WA UGAWAJI MADAWATI KWA MAJIMBO MBALIMBALI NCHINI LEO, AWATAKA JKT NA MAGEREZA KUKAMILISHA HARAKA KAZI YA UTENGENEZAJI MADAWATI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi moja ya madawati, Mbunge wa Ilala Mussa Azzan Zungu ambaye aliyapokea madawati kwa niaba ya Wabunge wa majimbo mbalimbali nchini, katika hafla ya mpango wa ugawaji madawati kwa majimbo mbalimbali nchini, iliyofanyika leo kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, leo.
 ------------------------------------------------
DAR ES SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezindua mpango wa ugawaji wa madawati yanayotengenezwa kutokana na fedha zilizotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kubana matumizi katika bajeti yake.

Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 13 Julai, 2016 katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam ambapo Rais Magufuli amekabidhi madawati 537 kwa mbunge wa jimbo la Ilala Mheshimiwa Mussa Azan Zungu kwa niaba ya wabunge wa majimbo yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ambayo yatagawiwa idadi hiyohiyo ya madawati kwa kila jimbo.

Madawati hayo 537 ni sehemu ya madawati 61,385 ambayo yametengenezwa katika awamu ya kwanza na yatafuatiwa na madawati mengine 60,000 yatakayogawiwa katika awamu ya pili na yote kwa ujumla yatagharimu shilingi bilioni 4 ambazo zilitolewa na Bunge tarehe 11 Aprili, 2016 baada ya kubana matumizi katika bajeti yake, ikiwa ni kuitikia wito wa Mhe. Rais John Pombe Magufuli.

Mikoa itakayonufaika katika awamu ya kwanza ya ugawaji wa madawati hayo ni Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza wabunge kwa kutoa mchango huo na pia amewapongeza wadau wengine ambao wameitikia wito wake wa kuchangia madawati kwa lengo la kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini.

Rais Magufuli amesema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5 hali iliyosababisha upungufu wa madawati 1,400,000 lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa ambapo mpaka sasa zaidi ya madawati 1,000,000 yametengenezwa.

Aidha, Dkt. Magufuli amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza kuongeza kasi katika utengenezaji wa madawati ili yakamilike haraka na kuanza kutumika.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa kamati ndogo ya tume ya huduma za bunge, Viongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Bunge.

0 comments:

Post a Comment