HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE SHEREHE ZA MAKABIDHIANO YA MAJENGO YA HOSPITALI ZA MNAZI MMOJA, SINZA NA RANGI TATU, TAREHE 11 DESEMBA, 2012


Mheshimiwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Balozi wa Serikali ya Jamhuri ya Korea;
Waheshimiwa Wabunge na Madiwani;
Viongozi na Watendaji wa Serikali;
Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mabibi na Mabwana:
Nakushukuru sana Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzako wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika tukio hili muhimu la makabidhiano ya majengo yatakayotumika kama vituo vya kutolea huduma ya afya kwa akina mama wajawazito na watoto katika Hospitali za Mnazi Mmoja, Sinza na Mbagala Rangi Tatu. Pamoja na majengo hayo leo tutakabidhiwa pia magari matatu ya wagonjwa na vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kutolea huduma kwenye vituo hivyo. Hii ni hatua kubwa katika jitihada za Serikli yetu za kuboresha afya za akina mama na watoto katika mkoa wa Dar es Salaam. Sasa tumeongeza uhakika wa kupata huduma zilizo bora zaidi kutoka kwenye vituo hivi.
Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na wananchi wote kwa ujumla, napenda kutoa shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Lee-Myung-bak, Rais wa Jamhuri ya Korea (Korea Kusini) pamoja na serikali yake kwa zawadi hii kubwa waliyotupatia. Sina shaka ye yote kuwa vituo hivi vitasaidia juhudi zetu za kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto. Hatuna neno zuri la kushukuru isipokuwa kusema asanteni sana.  
Gharama zote za mradi huu, ikiwa ni pamoja na majengo, vifaa na mafunzo kwa watoa huduma, ni shillingi bilioni 6.76  fedha ambazo ni msaada  kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea. Kabla ya msaada huu vituo vilikuwa havina magari ya wagonjwa, huduma za uzazi, upasuaji, na maabara zilikuwa hafifu na vyumba vya kutoa huduma vilikuwa vichache.  Kwa jumla mazingira ya kazi yalikuwa siyo mazuri sana na mambo yote hayo sasa yamerekebishwa na huduma zinazotolewa ni bora kuliko ilivyokuwa mwanzo. Kwa kweli marafiki zetu hawa wametuonesha upendo mkubwa na urafiki usio kifani. Bila shaka wamethibitisha ule usemi usemao: Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli. 
Ndugu wananchi;
Tangu nchi yetu ipate uhuru mwaka 1961  na kufanya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, Serikali yetu katika awamu zote imefanya na inaendelea kufanya juhudi kubwa za kuboresha huduma ya afya ili iwafikie Watanzania wengi zaidi na kwa gharama nafuu. Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani mwaka 2005 iliendeleza juhudi hizo bila ajizi. Tulianza kwa kuipitia upya Sera ya Afya ya Mwaka 1990 kwa lengo la kuihuisha ili iendane na changamoto za sasa zinazoikabili sekta ya afya. Matokeo ya zoezi hilo ni kuasisiwa kwa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (2007-2017), kwa kifupi MMAM.
Ujenzi wa vituo hivi ni matokeo ya utekelezaji wa Mpango huo kabambe wenye lengo kuu la kuongeza kasi ya uendelezaji na uboreshaji wa huduma ya afya kwa kujenga na kuimarisha hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini. Kazi hiyo tumeianza na tunaendelea nayo vizuri. Tunataka watu wasitembee zaidi ya kilomita tano kufuata huduma ya afya.  Aidha, tunaendelea kuboresha huduma zinazotolewa katika hospitali za Wilaya, Mikoa, Rufaa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Tunafanya hivyo nchi nzima kwa kushirikiana na wananchi, mashirika ya kijamii hasa ya dini, watu binafsi na washirika wetu wa maendeleo waliopo ndani na nje ya nchi yetu. 
Ndugu wananchi;
Wote mtakubaliana nami kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una changamoto ya pekee katika utoaji wa huduma ya afya kwa wakazi wa Jiji. Mkoa wa Dar es Salaam una watu wengi kuliko mikoa yote nchini.  Kuna wagonjwa wengi kutoka hapa Mkoani na wengi huja ama wenyewe au kuletwa Dar es Salaam kwa matumaini ya kupata huduma bora ya afya.  Hali hii inasababisha msongamano mkubwa katika hospitali za Serikali na  za binafsi zilizopo Jijini hapa. 
Kwa kutambua ukweli huu na kwa nia ya kupunguza adha  wanayoipata wagonjwa, Serikali imekuwa inafanya jitihada kuongeza hospitali, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.  Pia tunaongeza vifaa tiba, majengo ya kutolea huduma na idadi ya wataalam wa afya.  Kama nchi inayoendelea, uwezo wetu si mkubwa sana kutosheleza mahitaji yote.   Hiyo ndio sababu kubwa iliyonifanya mimi kuomba msaada Serikali ya Jamhuri ya Korea nilipoitembelea nchi hiyo mwaka 2006.  Bahati nzuri wakakubali kutujengea majengo haya tunayokabidhiwa leo yenye maabara za kisasa na kutuongezea vifaa tiba vya kisasa na magari matatu ya wagonjwa. Ndugu zetu hawa pia wametupatia mkopo ambao tunajenga hospitali kubwa ya kisasa kule Mloganzila, Kinondoni.  Hospitali hiyo itatoa huduma na kutumika kufundishia wanafunzi wa udaktari, uuguzi na taaluma nyinginezo za afya.  Tumeamua kukijengea Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili makazi yake mapya pale Mloganzila ili kuongeza uwezo wa kufundisha wanafunzi wengi zaidi ili tujitosheleze kwa mahitaji ya wataalamu wa afya.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa;
Ni kweli, ukilinganisha na tulivyokuwa huko nyuma, kwamba tumepiga hatua nzuri kufikia Malengo ya Millenia ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza vifo vya watoto na akina mama vinayotokana na matatizo ya uzazi.  Idadi ya vifo vya watoto wachanga imepungua kutoka 99 mwaka 1999 hadi 51 mwaka 2010 na vifo vya walio chini ya miaka mitano imepungua kutoka 147 hadi 81 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai. Kwa upande wa akina mama wajawazito idadi ya vifo imepungua kutoka 578 hadi 454 kwa kila uzazi salama 100,000. Lakini wastani wa watoto 562 (wachanga  na walio chini ya miaka mitano) na akina mama 23 kufariki kila siku ni kubwa mno. 
Tunaweza kupunguza zaidi vifo hivyo.  Ni vifo vinavyoweza kuepukika kwa kuongeza vituo vya kutolea huduma ya mama na watoto na kuboresha huduma itolewayo kama tufanyavyo leo. Hivyo nawaomba wadau wote wajitokeze kwa wingi kuunga mkono juhudi za Serikali za kupanua na kuboresha huduma ya afya nchini.  Hii itawafanya Watanzania wawe na afya bora na kuwezsha nchi yetu kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2015.  Ushirikiano wa wadau wote ni  muhimu sana katika kufanikisha azma hii.  Hapa nina maana ya Serikali, wananchi, watu binafsi na washirika wetu wa maendeleo kama tufanyavyo leo.  Tukiiachia Serikali pekee itachukua muda mrefu.  
Napenda kutumia nfasi hii kurudia wito wangu niliowahi kuutoa mwaka 2007 kwa  Manispaa zote tatu za Dar es Salaam kujenga hospitali na vituo vya afya vikubwa katika maeneo yao mbalimbali  ili kuzipunguzia mzigo hospitali zilizopo  sasa za Temeke, Amana na Mwananyamala.  Hali kadhalika narudia wito wangu kwa Halmashauri za Miji ya Makao Makuu ya Mikoa kujenga hospitali zao ili kuiacha hospitali ya Mkoa iwe ya Rufaa kwa Wilaya zote za Mkoa husika.  Mimi na wenzangu serikalini tunaahidi kutoa ushirikiano kwa wadau wote ili kuhakikisha kuwa huduma ya afya nchini inazidi kuboreka. Tunapenda kuona ahadi yetu ya maisha bora kwa kila Mtanzania ambapo upatikanaji wa huduma bora ya afya ni sehemu muhimu, inaendelea kutekelezwa. 
Tutaendelea kuongeza fedha kwenye bajeti ya serikali kwa ajili ya sekta ya afya ili vituo vya kutoa huduma viongezeke na kumudu majukumu yao ipasavyo. Tutaendelea kuongeza nafasi za masomo kwa wataalam mbalimbali wa afya ili idadi yao iongozeke na kuziba pengo lililopo. Kwa kufanya hivyo  mfumo wa utoaji wa  huduma ya afya  na miundombinu itaimarika zaidi na afya za watanzania zitaboreka zaidi. Tuna imani kuwa vifo vya watoto na akina mama vitapungua zaidi; magonjwa yatazidi kudhibitiwa na watu wengi watakuwa na uhakika wa kuishi maisha marefu zaidi kuliko ilivyo sasa.
Ndugu wananchi;
Sasa majengo haya katika hospitali za Mnazi Mmoja, Sinza na Rangi tatu yamekamilika. Nawaomba akina mama watumie vituo hivi kupata huduma ya uzazi salama. Waache kujifungulia majumbani, ni hatari kwa usalama wa mama na mtoto. Lolote linaweza kutokea. Vilevile, nawaomba madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa hospitali hizi watunze majengo haya na kutumia vizuri vifaa tiba na magari ya wagonjwa kwani bila ya kufanya hivyo baada ya muda si mrefu huduma zitadorora.  Halmashauri zitenge fedha za kutosha za uendeshaji wa hospitali, vituo vya afya na zahanati zake.  Mazingira ya kazi katika zahanati zetu hizo tatu yameboreshwa na vitendea kazi na vifaa vimeongezwa. Hakuna sababu ya kushindwa kutoa huduma kwa kiwango cha hali ya juu. Mshindwe wenyewe!
Kabla ya kumalizia napenda  naishukuru tena serikali ya Jamhuri ya Korea kwa msaada mkubwa waliotupatia. Balozi wao yupo hapa. Namwomba atufikishie salamu  na shukrani zetu nyingi kwa Rais na watu wa Jamhuri ya Korea. Tunawashuru sana kwa ukarimu wao. Tunaomba tuendelee kushirikiana pamoja katika kuboresha sekta ya afya na maeneo mengine.  

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa;
Ndugu wananchi;
Baada ya kusema maneno hayo machache, sasa nipo tayari kufanya kazi iliyonileta ya kupokea majengo haya na kuyafungua rasmi. 
Asanteni kwa kunisikiliza.