HOJA MTAMBUKA: KAMA PINDA AMEFUNGULIWA KESI KWA KUSEMA 'UTAPIGWA TU', VIPI ALIYETISHIA KUMWAGA DAMU?

Na Charles Charles
KITUO cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC) kikishirikiana na Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), kimemfungulia mashtaka Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Kayanza Pinda kufuatia kauli aliyotoa bungeni hivi karibuni dhidi ya wakorofi wachache wanaofanya vurugu nchini, kisha wanakaidi maagizo wanayopewa na vyombo vya dola ya kukatazwa wasifanye hivyo kwa kwenda kinyume chake.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Hellen Kijo Bisimba ndiye alifungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Alhamisi iliyopita huku Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa Kituo hicho, Harold Sungusia naye akimtaja Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kwamba ni mshtakiwa wa pili.

Mashtaka hayo yanadai kuwa kauli ya Pinda inakiuka Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Toleo la 2005 inayotumika sasa, kesi ambayo LHRC na TLS wanatetewa, kuwakilishwa au kushauriwa na jopo la mawakili 20 akiwemo aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha siasa cha NCCR – Mageuzi, Dk. Ringo Tenga.

Tayari Dk. Tenga amekaririwa na gazeti moja litolewalo kila siku nchini (siyo Uhuru) akisema wamezingatia zaidi sheria na haki za msingi za binadamu huku kauli ya Pinda iliyotolewa hadharani ikizihatarisha.

Akizungumza bungeni Juni 19, mwaka huu, Waziri Mkuu aliwaonya watu wanaofanya vurugu nchini, kisha hukaidi maagizo halali wanayopewa na vyombo vya dola kwamba waache.

“…Ukifanya fujo, (halafu) umeambiwa usifanye hiki ukaamua kukaidi utapigwa tu”, alisema alipokuwa katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yanayoulizwa kwake kila Alhamisi wakati wa vikao vya bunge na kuendelea:

“…Wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya sheria. Sasa kama wewe umekaidi (maagizo halali ya vyombo vya dola) unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndiye jeuri zaidi (polisi) watakupiga tu kwa sababu hakuna namna nyingine…”

Hayo ndiyo maneno ya Pinda yaliyosababisha aburuzwe mahakamani na LHRC na TLS huku Dk. Hellen Kijo – Bisimba, mmoja kati ya wanaharakati wanaosimama kidete mara kwa mara ili kuipinga serikali na viongozi wake akisema kuwa lazima Waziri Mkuu huyo ashughulikiwe kwa kuvunja Katiba ya nchi hii.

Nawaunga mkono LHRC na TLS kwa kuthibitisha jinsi gani walivyo mstari wa mbele katika uteteaji wa sheria, kulinda Katiba na haki za Watanzania ikiwemo Ibara ya 13(1) iliyotumika kumfungulia mashtaka hayo Pinda inayosema ifuatavyo:

“Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria” (mwisho wa kunukuu).

Mbali na hiyo, Ibara ya 14 pia inaeleza kwamba “kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria”.

Nimesema ninawaunga mkono LHRC na TLS kwa kutimiza kwa vitendo wajibu wao wa kutetea Watanzania na binadamu wengine, lakini sikubaliani kwa namna zote na ubaguzi unaozingatia maslahi ya kisiasa kuwa nani afunguliwe mashtaka ama nani asiguswe kwa vile huenda tu ni mwenzao!

Kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 uliokirejesha madarakani tena Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk, Wilbroad Slaa alitangaza kuwa asingekubaliana na matokeo yaliyotarajiwa kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akidai hayakuwa yenyewe.

Naomba ieleweke kwamba sina kinyongo naye chochote kwa kutishia kufanya hivyo maana ilikuwa haki yake, lakini nafahamu pia kuwa alikuja na madai hayo kwa sababu ya taharuki itokanayo na kuchanganyikiwa akilini.

Hakuamini kushindwa katika kinyang’anyiro hicho cha juu zaidi kuliko vyote vya kisiasa kwa kuzingatia Ibara ya 33(1) – (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alichanganyikiwa kwa sababu alikuwa amejipotosha mwenyewe na kupotoshwa kwa siku nyingi kabisa kwa kuitwa Rais mtarajiwa au Mkuu wa Nchi ajaye, Kiongozi wa Serikali na pia Amiri Jeshi Mkuu wa Tano wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Katika kikao chao na waandishi wa habari siku chache tu baada ya uchaguzi huo mkuu wa mwaka 2010, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na Dk. Slaa kwa pamoja walitishia kuwa endapo aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete angetangazwa kuwa mshindi ungetokea umwagaji wa damu dhidi ya Watanzania ambao ni pamoja na watoto wasiojua lolote wala chochote.

Walisema akitangazwa kuwa rais kwa awamu ya pili, Kikwete naye asingeweza kumaliza miaka mitano akiwa madarakani, kauli inayokiuka Ibara ya 38(1) ya Katiba na Ibara ya 3(14) ya Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 1979 iliyofanyiwa marekebisho na kuwa Ibara ya 9(15) Mwaka 1984.

Walijua wanakiuka Ibara ya 41(6) ya Katiba ya nchi yetu na Ibara ya 5 ya Sheria Na. 20 ya Mwaka 1992 na Ibara ya 10 ya Sheria Na. 34 ya Mwaka 1994 zinazohusu Utaratibu wa Uchaguzi wa Rais.

Ndivyo pia LHRC na TLS zinavyofahamu kushinda hata mimi, lakini hazifanya lolote ama kusema chochote achilia mbali kwenda kuwafungulia mashtaka ya kuvunja Katiba ya nchi yetu kama zilivyofanya dhidi ya Pinda.

LHRC na TLS zinajua ukweli kuwa Pinda alitoa kauli ile bungeni akiwatetea Watanzania wanaofanyiwa vurugu na kikundi cha wakorofi wachache, na kwamba alifanya hivyo kwa kuzingatia Ibara ya 14 – 15(1) za Katiba na Ibara ya 6(15) ya Sheria ya Haki ya Kuishi ya Mwaka 1984.

Nimesema tokea mapema kuwa nawaunga mkono LHRC na TLS kwa kuthibitisha kwa vitendo wajibu wao wa kuwatetea Watanzania na binadamu wengine, lakini katika kesi yao dhidi ya Pinda siwaungi mkono kwa sababu naamini kabisa kwamba wanachofanya sasa ni kupotosha ukweli kuhusu vifungu hivyo vya Katiba ya nchi hii!

Siwaungi mkono kwa sababu inanituma akilini kuwa kesi hiyo imefunguliwa kwa misingi ya kisiasa zaidi, chuki zao dhidi ya CCM na juhudi za makusudi za kutaka kuwatisha viongozi wa serikali yake ili kuwatia hofu isiyokuwa na maana wala faida yoyote; na pia wanajitahidi kwa nguvu zao zote, juhudi na maarifa yao yote kuvisaidia baadhi ya vyama vya siasa hasa Chadema kwa kutumia elimu yao ya sheria.

Fikiria kwa mfano viongozi wa Chadema walivyotangaza kwamba Kikwete asingedumu madarakani kwa ile miaka yake mitano ya sasa, lakini LHRC wala TLS hawakuonekana popote kwa kusema chochote midomoni mwao ama kufanya lolote kwa namna yoyote.

Wote walibaki kimya utadhani hawakuwepo kabisa Tanzania wakati kumbe wangeweza kuwafungulia mashtaka ya kutishia maisha ya rais, kuhatarisha amani na usalama wa taifa na kutaka kuipindua serikali kabla ya mwaka 2015 kinyume cha Ibara ya 38(1) ya Katiba yetu.

Hakuna yeyote kati ya LHRC na hata TLS aliyesema wala kufanya chochote, badala yake walijifanya kwamba eti hawaangalii kabisa matangazo yoyote ya televisheni, hawasikilizi redio na hawasomi magazeti na hata mtandao wowote ule wa kijamii iwe facebook, jamii forum, google na kadhalika na kwa hiyo hakuna yeyote kati yao aliyekuwa akifahamu kitu chochote kuhusiana na vitisho hivyo vya hatari kwa nchi yetu!

Mbali na kauli hizo za kutishia umwagaji wa damu na kukiuka Katiba kwa makusudi na waziwazi, Mbowe aliwatangazia tena wananchi kwamba Tanzania isingetawalika mwaka huu wa 2013.

Alikuwa akiishinikiza serikali kuwa itekeleze matakwa ya Chadema, na kwamba isipofanya hivyo Tanzania ingeingia katika wimbi kubwa la mauaji ya halaiki, utekaji nyara au mateso mengine yoyote ili mradi chama hicho kinakidhi matakwa yake ya kisiasa.

Nashangaa kwamba kumbe kuna LHRC na TLS zinazoijua vizuri Katiba ya nchi yetu, kuiheshimu pamoja na kuizingatia sana, lakini zote hazikumfungulia mashataka Mbowe wala Dk. Slaa kwa sababu tu huenda ni viongozi wao kiitikadi.

Pamoja na kutojua nani atashinda katika kesi hiyo inayotarajiwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu ambao bado hawajatajwa, lakini kwa hukumu yoyote nitaendelea kumuunga mkono Waziri Mkuu Pinda kuwa aliitoa kauli ile kwa ajili ya maslahi ya Watanzania wote, na pia alifanya hivyo kwa kuzingatia Ibara ya 13(1) ya Katiba ya nchi hii.

Kama LHRC au TLS wanadhani alikosea na ndiyo maana wakamfungulia mashtaka, mimi siku zote nitahoji hadi waniambie ni nani aliyekiuka haki hizo za binadamu kati ya Waziri Mkuu huyo katika upande wa kwanza na Mbowe ama Dk. Slaa katika upande wa pili.

Kama ni kweli kuwa Pinda alikiuka Ibara ya 13(1) alipokemea watu wanaofanya vurugu na kutojali wanapoonywa kwamba wakiendelea watapigwa, hakika hata iweje sikubaliani kwa namna yoyote ile na LHRC wala TLS ziliposhindwa kumfungulia mashataka Mbowe wala Dk. Slaa kwa kutishia kumwaga damu na kusema Tanzania haitatawalika mwaka 2013!

Bila kufanya hivyo hata kama Pinda atafungwa endapo atashindwa katika kesi hiyo imani yangu itaendelea kuziona LHRC na TLS kwamba zinafanya ubaguzi kwa kuangalia itikadi za kisiasa.

Nitaendelea kuzihoji kama zinaunga mkono umwagaji wa damu, vurugu na kutotii mamlaka iliyopo madarakani au zinataka Tanzania pia isitawalike kama ilivyo Iraki, Sudan, Somalia, Pakistani, Afghanistan au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako mauaji ya halaiki ni jambo la kawaida.

Kama LHRC na TLS zinaiona kauli ile ya Pinda aliposema ukijifanya jeuri “utapigwa tu” inakiuka Ibara ya 13(1) ya Katiba na kufunguliwa kesi; vipi Mbowe aliyetishia kumwaga damu kwa kusema Tanzania haitatawalika mwaka 2013?

Kila Mtanzania wa kweli aingie kichwani mwake na kujiuliza mwenyewe!

Mwandishi wa makala hii ni Katibu wa CCM wa Wilaya ya Shinyanga Mjini

0 comments:

Post a Comment